Friday 16 March 2018

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA UFUGAJI WA SAMAKI KWENYE MABWAWA NA Godfrey Christopher Sway Aquaculture Sokoine university of Agriculture


 MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA UFUGAJI WA SAMAKI KWENYE MABWAWA.
katika makala hii tunazidi kufahamishana fursa zinazotuzunguka,ambazo kwa  uthubutu wa  mtu yeyote katika jamii yetu anaweza kuzichukulia hatua na kuzifanyia kazi.

Kutokana na mahitaji ya samaki duniani kuzidi kushamiri kwa sababu ya ongezeko la wingi wa watu na uhaba wa sehemu zenye  maji ya asili kama mito na maziwa kwa samaki wa maji baridi pia bahari kwa samaki wa maji chumvi,kumezidi kuhamasisha watu kungundua namna za kuweza kujipatia kitoweo hichi haswa ikichochewa na hamasa inayotokana na faida ya nyama  nyeupe ya samaki katika mwili na afya ya binadamu.

Ufugaji wa samaki kwenye mabwawa ya kuchimbwa umekuwa ukishamiri duniani kote inchi kama Thailand, China, Indonesia, Peru, Norway Denmark n.k

Niwazi tumeona baadhi ya inchi nyingi zikizidi kuzalisha nafasi nyingi za ajira kwa shughuli hizi pamoja na kukuza kipato cha mhusika mmoja mmoja, jamii flani na taifa kwa ujumla.

Katika kuiangalia fursa hii tutaangalia vipengele ambavyo kwa kufatilia wataalamu na wafugaji mbali mbali tumegundua vitasaidia sana kutoa mwanga kwenye fursa hii na kuzidi kutoa hamasa si ya kusoma tu makala mbali mbali ya ujasiriamali na tafiti za biashara bali pia kuchukua hatua stahiki katika kufanikisha malengo yako.


Vipengele hivyo ni:
  • Eneo,
  • Maji
  • Aina za mabwawa,
  • Ujenzi wa Bwawa,
  • Mifumo ya ufugaji wa Samaki,
  • Ufugaji wa samaki,
  • Maadui wa samaki ni,
  • Ubadilishaji wa maji,
  • Ulishaji wa samaki,
  • Mtaji,
  • Fursa zinazoweza jitokeza kwenye maji yanayofugia samaki,


ENEO
Katika ujenzi wa bwawa la samaki nikipengele ambacho kinatakiwa kuangalia sana.Ni mara chache  wahusika wamekuwa wakizingatia kigezo hichi.Swala la eneo linakuwa limebeba vigezo vingi sana kama :

  • mwinuko wa eneo husika ili kuzingatia swala la uingizaji na utoaji wa maji kwenye bwawa litakapokuwa limejengwa,
  • vyanzo vya maji katika sehemu husika,
  • Aina ya udongo katika sehemu husika.
  • ukubwa wa eneo husika,na mazingira yake kwa usalama wa zoezi zima la ufugaji wa samaki,
  • Fursa nyingine zinazoweza tumika kwa maji yanayokuwa yakibadilishwa kutoka kwenye bwawa. Fursa hizo ni kama kilimo na shughuli nyingine zenye uhitaji wa maji hayo.
Swala hili ni muhimu sana na tunashauri ni vyema kuwasiliana na wataalamu waliobobea kwenye maswala haya ya ufugaji wa samaki kabla ya kuamua kufanya biashara hii ya ufugaji.Wataalamu hao wanaweza kukupa ushauri mzuri wa jinsi gani uyajenge mabwawa ya samaki kulingana na hali ya eneo lako lilivyo na ukubwa wa eneo husika.

MAJI

Maji ni moja ya kigezo kikubwa sana kwenye biashara ya ufugaji wa samaki.
Kitaalamu tunasema maji ni kila kitu katika ufugaji wa samaki.

Yaani usipozingatia hapa basi ni ngumu kupata matokeo uliyoyatarajia.

Kwenye swala la maji ni vyema kufahamu yafuatayo:

  • Ni vyema kushirikisha wataalamu kama unataka kupata matokeo mazuri .Hii ni kutokana na ukweli kwamba ufugaji wa samaki wa maji baridi yaani maji yasiyokuwa ya baharini ni vyema wataalamu waweze kupima na kucheki PH na ubora wa maji husika kama yanafaa kwa zoezi hili.Kigezo hichi kifanyike kabla hujaanza zoezi la ujenzi wa bwawa.
  • Pindi utakapokuwa ushaanza zoezi la ufugaji wa samaki ni vyema kabisa kuwasiliana na wataalamu ili waweze kukupa utaratibu sahihi kwa ajili ya kupima Oxygen kama inatosha kwenye bwawa husika hii inachangia sana katika uhai na maisha ya samaki bwawani.
  • Ni vyema kupata utaratibu wa namna ya kupima jotoridi kwenye maji ya bwawa lako hii inatokana na mazingira yetu ya Tanzania kuwa na vipindi mbali mbali katika mikoa tofauti.Sababu hii ni vyema kuzingatia sababu nayo ni sababu kubwa katika ukuaji wake.
  • Sababu hizi zitakusaidia endapo unaanza ufugaji wa samaki ni wakati gani mwafaka wa kubadili maji na kwa kiasi gani kubadili maji yaliyoko kwenye bwawa lako.

kwa utafiti wetu tumeona ni vyema kuhusisha wataalamu ili wakupe mbinu sahihi kwa ajili ufugaji bora wa samaki kibiashara utakaoambatana na matokeo bora.

AINA ZA MABWAWA

 Zipo aina nyingi za mabwawa ila kwa lugha rahisi tutakupa ufafanuzi mdogo ambao ni:

  • Yapo mabwawa ya kuchimbwa chini na kama ardhi yake inatwamisha maji basi linachimbwa tu baadae zinafata taratibu nyingine za zoezi la kuandaa uwekaji wa samaki.
  • Yapo mabwawa ya kuchimbwa na kujengewa yamkini kuta zake au kujengewa bwawa zima.
  • Yapo mabwawa mengine ambayo yanajengewa kuanzia usawa wa ardhi ambayo mara nyingi huwa duara. Kitaalamu yanaitwa concrete tanks.
  • Tunashauri pia kuwashirikisha wataalamu watakupa mwanga wa namna wa bwawa la kujenga kigezo kikiwa ni eneo ulilonalo, aina ya udongo ulionao,mtaji wakuanzia na vigezo vingine vidogo.


UJENZI WA BWAWA

Ujenzi wa bwawa unatofautiana kulingana na eneo husika,ukubwa wa mradi unaotaka kuuweka,aina ya udongo,maadui wa samaki walioko kwenye eneo husika.

katika kukupa mwanga wa fursa hii tutakupa hatua kadhaa zinazolenga kwenye ujenzi wa bwawa.

Hatua hizo ni:

  • Kina cha bwawa la samaki mara nyingi hutofautiana Kati ya maingilio ya maji na matoleo ya maji ambapo maingilio ya maji huwa na kina kifupi zaidi kulinganisha na matoleo ya maji ambapo matoleo huwa na kina cha mita  moja na nusu (1,5) ila mara nyingi wataalamu wanasema inategemeana na ukubwa wa bwawa la samaki,
  • Mabwawa mengi kuta zake hujengwa kwenye mwinuko wa wa nyuzi 45 hii inasaidia kurahisisha uvunaji,kuzuia mmomonyoko wa kuta  kwenye bwawa,
  • Kama bwana ni la kuchimba basi ujenzi hufanyika kulingana na maelekezo ya wataalamu ili kuzingatia aina ya udongo iyoko sehemu husika.Ingawa ni vyema kufahamu kama ardhi inapitisha maji basi unaweza tumia polythene sheet ili kuzuia maji yasipotee pia kama ni kujenga basi ni vyema kufahamu kwamba utumiaji wa matofali

Tunashauri ujenzi huu wa bwawa ni vyema kushirikisha wataalamu ili kupata matokeo mazuri kibiashara.

MIFUMO YA UFUGAJI WA SAMAKI

Katika ufugaji wa Samaki kwenye mabwawa mifumo ya ufugaji wa Samaki mayo imegawanyika katika sehemu kuu Tatu;

Mfumo wa extensive: Mfumo huu unahusisha utumiaji wa vitu asili Kama chakula kinachopatikana  ndani ya maji,uangalizi wake ni mdogo,pia uwezekano wa Samaki kushambuliwa na magonjwa pia ni mdogo,uwekezaji wake ni mdogo na uvunaji wake pia ni mdogo

Mfumo wa semi intensive:
Mfumo huu unahusisha teknolojia ya Kati ambayo chakula cha asili ndani ya maji na urutubishaji wa bwawa una husika kwa kiasi fulani,pia chakula cha ziada kina ongezwa, uhudumiaji wake kwa ujumla ni wa saizi ya kati kama uangalizi, udhibiti wa magonjwa , uwekezaji wake na pia uvunaji wake ni wa wastani

Mfumo wa intensive:
Mfumo huu unahusisha utumiaji wa teknolojia ya hali ya juu Sana ambayo urutubishaji wa bwawa unatumika, pia chakula kinachotumika ni kile kilicho fanyiwa kanuni za kisayansi ili kupata uwiano halisi wa virutubisho vyote vinavyohitajika kwa ukuaji wa samaki,uhudumiaji wake ni wa hali ya juu Kama kuangalia ubora wa maji kila wakati,huduma zote hufanyika kwa ustadi wa hali ya juu sana Kama kudhibiti magonjwa,pia uwekezaji na mavuno yake ni ya hali ya juu sana

UFUGAJI WA SAMAKI

Kipengele hiki ni miongoni mwa vipengele mama katika ufugaji wa samaki kwani kitakuongoza kujua uamue ufuge aina gani ya ufugaji ili kuweza kujipatia kipato,kujipatia kitoweo na kukidhi matakwa ya mahitaji ya samaki kwa wateja wako .Ufugaji Upo wa aina mbili:

Monoculture: ufugaji huu unahusisha aina moja ya samaki kukaa katika bwawa pia waweza kufanyika katika maji baridi au maji ya chumvi.Tukichukulua mfano wa maji baridi waweza kufuga sato(tilapia species) tuu katika bwawa au kambale(clarius species)

Polyculture:
aina hii ya ufugaji unahusisha kuchanganya aina mbili au zaidi kwenye bwawa moja .tukichukulia mfano wa maji baridi waweza kufuga samaki aina ya sato(tilapia)  na samaki aina ya kambale(clarius) kwenye bwawa.

MAADUI WA SAMAKI
Katika ufugaji wa samaki kwenye mabwawa ya samaki changamoto kubwa ni maadui wa samaki.Zipo njia nyingi za kujikinga na changamoto.

Maadui wa samaki kwenye mabwawa ni:
  • Vyura
  • Kenge
  • Nyoka
  • Ndege

Tumegundua baadhi ya maadui wakubwa wa samaki kwenye mabwawa ni hao walio orodheshwa hapo juu.Kujikinga na maadui hao ni vyema yafanyike yafuatayo:

Kujikinga na vyura ni vyema kuhakikisha unaweka uzio wa fensi ya waya kuzunguka bwawa lako kama unauwezo wakufanya hivyo,fensi hii hakikisha iwe ya vitundu vidogo ili kuweza kuwa kizuizi kwa jamii hii.

Jamii ya Kenge pia inaweza kuzuiwa na aina hii ya fensi na ni vyema kuhakikisha huachi uotaji wa kichaka kikubwa karibu na eneo la bwawa ili kuepusha mazalia na maficho ya viumbe hawa.

Kwa kizuizi cha ndege ingawa wengi wanatumia urutubishaji wa maji ya samaki kwa kutumia mbolea ili kusaidia pia katika chakula na kinga ya samaki dhidi ya maadui wake kama ndege,utaratibu wa kufunga kamba zinazokuwa na umbali mdogo unaoachanisha nyuzi na nyuzi.

Hii itatengeneza mazingira magumu kwa jamii zozote za ndege kuingia kwenye bwawa na kunyakua samaki.

Ni vyema kuhakikisha unaweka wavu wa fensi mkubwa na mlango kama eneo lako halina usalama ili kuondoa hatarishi za maisha kwa watoto au binadamu wengine ili wasitumbukie kwenye bwawa.

Ni vyema kuwasiliana na wataalamu wa samaki ili kupata ushauri zaidi kwa ajili ya kujilinda na maadui wengine na kuweza kupata matokeo mazuri.

UBADILISHAJI WA MAJI

Kama ilivyo ada maji ni kila kitu kwa samaki, tumegundua pia zoezi la kubadili maji linabidi lizingatiwe sana ili kupata matokeo mazuri. imegundua kuwa vipo vigezo vingi vinavyotakiwa kuangaliwa kama ubora wa maji, joto la maji husika kulingana na eneo na hali ya hewa ya eneo husika, uchafu wa maji kutokana na chakula na alkalinity na acidity ya maji.ni vyema kuvifahamu vitu hivi kitaalamu ili kujua wakati sahihi wa kubadili maji.Suluhisho la zoezi hili ni kushirikisha washauri wa maswala la ufugaji wa samaki na wataalamu wa kitengo hichi.

ULISHAJI WA SAMAKI

Wataalamu wengi wana njia (formula)  tofauti tofauti za ulishaji wa samaki lakini vigezo vikubwa vikiwa ni ukubwa wa samaki husika,idadi ya samaki kwenye bwawa husika,asilimia za uwezekano wa samaki kuishi,na kasi ya kula. Kitaalamu uwiano mzuri wa samaki na chakula anachokula ni asilimia 10% ya uzito wao kwa vifaranga wadogo kabisa na asili 5% ya uzito wao kwanzia wakiwa na mwezi mmoja na kuendelea.
 Ni vyema kuhakikisha samaki wanapewa kiasi wanachomaliza kipengele cha uzito kikizingatiwa,hii itasaidia kupunguza chakula kubaki kwenye bwawa na kusababisha uchafuzi mkubwa wa maji na ikichangia kupoteza gharama kubwa za ulishaji.


Wataalamu wanashauri kuwa ni vyema kutowapa chakula wakati wa mvua,wakati wa usiku  na wakati wa wingu zito hii itasaidia kuto kupoteza chakula bure na kupunguza gharama kwa sababu wakati huu samaki ulaji wao ni mdogo sana.

MTAJI

Kipengele hichi ndicho kinawapa changamoto wapenda fursa. Inashauri ni bora kujitadhimini mtaji wa kiasi gani unao na una lengo la kuzalisha kiasi gani na kufahamu gharama za uendeshaji.Maswala ya kuwashirikisha wataalamu itakusaidi kufahamu ni gharama gani zitakazo kwenda kwenye:

  • Mpangilio wa eneo,
  • Upimaji wa maji,
  • Uchimbaji wa visima kama kunaulazma,
  • Upatikanaji wa maji kama ni kutoa kutoka kwenye vyanzo vya maji,
  • Uchimbaji wa bwawa,
  • Ujenzi wa bwawa kama kuna ulazma,
  • Ujenzi wa vizuizi vya maadui wa samaki ili kuhakikisha usalama wa samaki mwenyewe na uwekezaji wa mwekezaji,
  • Gharama ya vifaranga kulingana na ukubwa wa bwawa,
  • Gharama za chakula cha samaki
  • Gharama za uendeshaji wa mradi wa samaki n.k
  • Kama mwekezaji ni vyema kufahamu vitu hivi ili kuweza kujua kwa makadirio gharama za uwekezaji ni kiasi gani na nini mategemeo yako kwenye uwekezaji wako.


FURSA ZINAZOWEZA JITOKEZA KWENYE MAJI YANAYOFUGIA SAMAKI
Katika kila fursa mara nyingi ukiangalia kwa makini kuna fursa nyingine.Nijukumu la kila mtu kuangalia kwa makini kila fursa changamoto inayojitokeza yamkini ni mwanzo wa fursa nyingine.

Maji yanayokuwa yanatolewa kwenye bwawa la samaki yanakuwa na virutubisho vingi katika umwagiliaji wa mazao mbali mbali.

Ni vyema kufahamu kwa kupima udongo wa eneo lako ili kufahamu mazao gani yanastawi vyema hii itakupa fursa ya kufanya kilimo kingine cha umwagiliaji kwa kutumia maji yanayobadilishwa toka kwenye bwawa lako.
 

Fursa hiyo inaweza kuwa ya kilimo cha:
  • Mapapi,
  • Maembe,
  • Migomba ya ndizi,
  • Nyanya,
  • Vitunguu,
  • Pilipili hoho,
  • Mboga mboga za majani n.k

Ni vyema kufanya upimaji wa udongo toka sehemu husika ili kujua fursa itakayo ambatana na ufugaji wa samaki nahii itasaidia kuweka maji yako safi kwa kigezo kwamba kama zoezi la umwagiliaji litakuwa ni la mara kwa mara basi maji yatakuwa yanatumika ya bwawani kupitia outlet uliyoijenga na kutumia inlet utakuwa unaongeza maji masafi.

Hii itasaidia kuweka na kudumisha maji yako yawe masafi zaidi.

3 comments:

  1. Asante sana kiongozi kwa elimu hii muhimu na adhimu. Kimsingi nimevutiwa sana na makala hii kiasi cha kushawishika kuanza mradi. Tafadhali naomba kuuliza maswali kadhaa kwa uelewa mzuri wa awali

    1. Je ni bwawa kiasi gani linatosha kwa samaki kiasi gani hususani aina ya Sato?

    2. Je iwapo bwawa ni la kuchimba na hakuna chanzo cha maji kingine ubadilishaji wa maji inakuwaje?

    3. Je ninaweza kufanya nini kama eneo langu ni la bondeni ambapo bwawa limechimbwa kwenye mkondo wa maji kurahisisha uvunaji wa maji wakati wa mvua kudhibiti uchukuliwaji wa samaki na maji yanayokimbia?

    Ninashukuru sana kwa majawabu mtaalam

    ReplyDelete
  2. How casino gambling is disrupting gambling culture
    Even with the launch of legal 딥 슬롯 online 먹튀 없는 사이트 casinos in the United 바카라마틴 States, casinos 바카라사이드배팅 will remain 1xbet online illegal, but are no longer safe. In the absence of Sep 30, 2020

    ReplyDelete